Asubuhi na mapema alipofika ofisini alianza kupekuapekua karatasi zilizokuwa mezani, alishindwa hata aanze kushughulikia kazi ipi kwanza. Alikusanya fomu kwa upande mmoja angalau apate nafasi ya kufanya kazi yake, alipokuwa anaendelea kupanga na kupangua yale makaratasi yaliyotapakaa mezani, aliona hatimiliki ya shamba.
"Kwani huyu hakuchukua hiki cheti chake!" Alijiuliza akiiweka kando na makaratasi mengine.
Aliichukua tena alipokuwa ameweka akaiangalia kisha kicheko kikamtoka, kilikuwa kicheko cha kujidhalilisha mwenyewe.
"Kweli dunia ina mambo yake," alijiambia akitikisa kichwa na kuikazia macho ile hatimiliki.
Alianza kukumbuka kilichotokea mpaka hatimiliki iliyokuwa mikononi mwake kufika pale ofisini.
Majuma mawili yalikuwa yamepita kutoka hatimiliki hiyo ilipofika ofisini mwake kwa njia ya kimabavu na kwa sababu ya wengine kunyimwa haki ili ifike pale ilipokuwa.
Akili ilimrejesha kortini mjini Zirala mbele ya hakimu Bw. Sizima, kijana Sumba akiwa amesimama kizimbani.
"Bw. Sumba, leo ni siku ya tatu mbele ya kikao hiki," Bw. Sizima alianza, "mara mbili mtawalia umekataa mashtaka, leo unakubali au la?"
"Bado nakata, siwezi kukubali ambacho sikufanya," yule kijana alimjibu kwa ushujaa, "mimi nilikuwa namtetea babu yangu."
"Kumtetea kwa njia ya kuzua rabsha mle ofisini?" Hakimu alimuuliza, "ulikuwa unamtetea kwani yeye ni mlemavu!"
Sumba aliinamisha kichwa akatabasamu, akainua tena na kumwangalia hakimu.
"Alikuwa amemzidia nguvu ewe bwana wangu."
"Sasa wewe ukaona una maguvu ya kipigana na mwenzio sio, ukajichukulia sheria mikononi."
"No your Majesty."
"Ripoti ambayo imenifikia baada ya uchunguzi kufanywa ni kuwa mlienda kudai hela ambazo mzee wako alikuwa ashalipwa, hayo ni kweli!" Hakimu alimuuliza akiwa amemkazia macho.
Badala ya kumjibu, Sumba alicheka kicheko kilichosikika mwisho wa jumba hilo, kila mtu akashtuka na kumwangalia aliyekuwa kando yake, kisha kwa pamoja macho yote yakaelekea kizimbani.
"I can see, you are going mad," hakimu alimwambia kwa hasira, "is that a laughing matter!"
"Nimekwambia ukweli mara ngapi? Sasa nimechoka," Sumba alimwambia kwa ukakamavu, "sina lingine ila kucheka tu. Najua ulikuwa ushanikatia hukumu hata kabla sijafika kizimbani ndo maana hata nikipinga sitabadili chochote. Unasema 'mi naenda kuwa wazimu, ila hiyo ni heri mtu pungwani kuwa kizimbani kuliko mwendawazimu mwenye tamaa kukalia kiti cha hukumu."
Bw. Siga alikumbuka jinsi hakimu alichukua faili iliyokuwa mbele yake kwa hasira baada ya kusikia yale, akamtupia jicho bwana Vura pale alipokuwa, akamtupia kijana kizimbani kisha mwisho akamwangalia babu yake Sumba.
"Kwa sababu ya kukosea korti heshima na bendera tukufu ya nchi; nimekukatia rufaa ya milioni ishirini na tano au shamba la babu yako," hakimu alitoa hukumu yake kisha akaondoka.
Yale yaliyotokea yalipompita akilini alichukua faili iliyokuwa kando kabisa na faili nyingine akalitia ndani ya mkoba kisha akaondoka.
Aliabiri gari kuelekea nyumbani kwa bosi wake, alipoangalia saa yake ya yalikuwa masaa ya adhuhuri, gari likikuwa limepakia mpaka nafasi ya nzi kupenya ikakosekana. Aliroa kwa jasho kwa sababu ya joto, baada ya kusafiri kwa saa nzima alitia nanga mbele ya lango la mdosi wake.
"Nitampata kweli...," alitia shaka kabla ya kubisha mlangoni. Alisikia ugomvi uliokuwa umepamba moto kati ya mume na mkewe.
"Tabia zako zimenichosha," alimsikia Bw. Vura akimwambia mkewe.
"Wewe nawe vivyo hivyo," alimsikia mkewe akimrudishia, "nitakuvumilia mpaka lini...heri tutalikiane."
"Hilo tu, si gumu kwangu au unafikiri talaka inanishtua. Mambo ya matisho nishapita."
"Si vitisho," mkewe alifoka, "ni mara ngapi nimekupata umefumaniwa nikakuokoa kwa sababu nakupenda, we unastahili mwenye nguvu za sumaku kukuvumilia...mimi na wewe yetu yamefika mwisho."
Alikuwa amesimama mlangoni dakika kumi akisikiliza ugomvi wao, alishangazwa na tabia na tabia za mkubwa wake, alikuwa akifikiri labda tabia yake ni kazini tu.
"Kama unataka talaka nisubiri papo hapo, usifikiri nitakupa kesho. Mke asiye na haya kutembea na vijana wadogo hirimo ya watoto wake."
"Naisubiria, leo sitarudi nyuma tena, mwanaume ambaye hana haya kutembea na wasichana wadogo wanaofaa kuwa waju...," mkewe alikatizwa na mbisho mlangoni.
Mkewe alimnyoshea kidole kumuonya, kisha akatoka nje kwenda kumuona aliyebisha mlangoni.
"Nafikiri hujasimama hapa kwa muda," alimwambia Bw. Siga akimkaribisha ndani.
"Ndo nafika sasa hivi," Bw. Siga alimdanganya mwenyeji wake, "nimempata lakini..."
"Ndiyo, karibu ndani."
"Asante, lakini labda umpe taarifa kwamba mgeni amemngojea ukumbini," Bw. Siga alimwambia akisonga kando, "yuko salama lakini!"
"Ndiyo, salama kabisa."
"Nafurahi nikisikia hayo, si vema kwa familia mara nyingi kuwa katika hali ya mifaraghano."
"Ni kweli, sijaona kibaya kwake."
Bi. Adimu aliingia ndani kumpasha mumewe habari akamuacha mgeni wao akielekea ukumbini. Alipofika mlangoni akimtazama mumewe, alimuona amefura kama mama-chura akacheka, kicheko kilimtoka cha hasira.
"Hebu niondokee," mkewe alimfukuza, "mwenzako anakungojea nje."
"Usifikiri yameishia hapa," Bw. Vura alimwambia, "bado nitarudi...na leo.'
"We nenda."
Bw. Vura alitoka akapita mpaka bafuni kunawa kisha akatoka kwenda kukutana na Bw. Siga, alitembea mwendo wa kinyonga akiangalia nyuma. Alikuwa amegombana na mkewe lakini alijua ndiye mkosaji na ugomvi huo alizua akijitetea.
***
Kama kawaida yake aliwawahi wote kuamka katika lile jumba lake, aliamka saa kumi na mbili za alfajiri akaanza kwa kufagia mbele ya jumba lao.
Alipomaliza kunadhifu nje ya jumba hilo ulikuwa mwendo wa saa moja kamili akaingia jikoni na kutoa vyombo, alisimama akashindwa pa kuanzia, vyombo vilitapakaa kote.
"Acha nikupe mkono," alisikia mwanawe akimwambia kando yake, "nenda kajishughulishe na kazi nyingine."
"Kweli wewe ni mvuvi wa kuamka, saa mbili inakaribia ndo mwanamke anaamka," mamake alimtania, "let me hope you were not like this in school."
"Lakini mama, naogopa baridi ya asubuhi," Labibu alimwambia akichota maji ya kunawa, "tena unajua nina mafua."
"Hiyo isiwe sababu, mwanamke unafaa kumtunza mumeo aamkapo apate ushashughuka kila panapohitajika au utapokonywa."
Bi. Tabasuri aliinuka akaondoka kuelekea jikoni, lakini alipofika mlangoni kifushi cha jifu kikamkumbusha kwamba hajafagia milki yake. Nje alipomuacha, Labibu alikuwa amesimama akiangalia vyombo bila kujua pa kuanzia.
Jua lilikuwa linaanza kuchomoza na jotojoto la miale yake kutua juu yake lakini aliogopa maji.
"Mum," alimuita mamake akiinama chini kuanza shughuli yake.
"Usianze umbea asubuhi, hebu kamilisha kwanza unachofanya, mazungumzo baadae."
"Siwezi kikusemea umbea, umetambua leo kuna kitu kisicho cha kawaida."
"Nini?."
"Mpaka sasa inaelekea saa mbili na baba haonekani."
"Usione umemeza tembe maumivu yakapungua umcheke aliye kitandani," mamake alimwambia akitoka nje, "nyie nyote ni wagonjwa na hakuna aliye heri ya mwenzake."
"Nkmejua sasa niondokapo nyie hubaki kunisimanga," sauti nzito ikimshtua Labibu ikitokea mlangoni, "mama na bintiye wanamsema mwenzao."
"Lakini hatujakusema mengi."
"Ni heri mfanye halahala, siku hii nimeitenga kwa ajili yenu, nataka angalau tutoke kama familia tuende tustarehe katika mojawapo ya hoteli za mjini."
"Naona shughuli zako za kila siku zikikaribia kukoma," mkewe alimpazia sauti kutoka jikoni.
Bw. Nadama hakushughulika kumjibu, aliondoka akaelekea bafuni. Labibu alianza kusafisha vyombo kwa haraka baada ya kusikia muondoko ambao babake alikuwa amepanga.
Baada ya kisebeho kuandaliwa mezani, walijumuika kama familia kushtaki njaa. Pale mezani, Labibu alikuwa amekisinzilia kikombe chake, mamake alimtupia jicho kisha akageuka na kumwangalia babake.
"Umemfanyia nini mwanangu mpaka akakaa kisanamu!" Bi. Tabasuri alimtupia mumewe lile swali akitaka kumuondokea mwanawe katika bahari ya luja.
"Mara ya mwisho kuwa na kikao cha kifamilia kama hiki ilikuwa lini!" Labibu aliuliza bila kumkusudia yeyote kujibu, "asante baba. Asante kwa ziara ya leo."
"Huna haja ya kunipa shukrani, leo nimeona angalau nitembee na familia yangu kwa sababu sina kazi nyingi ofisini."
Walikunywa kwa furaha wakila gumzo, lakini Labibu alikuwa na mawazo yaliyomsumbua akilini, alijaribu kujisahaulisha kwa kujizamisha katika maongezi yaliyonoga kati ya wazazi wake bila mafanikio. Baada ya kustaftahi, walijianda kisha wakaondoka kuelekea mjini.
Pale ambapo Bi. Tabasuri alikuwa ameketi alipoangalia nyuma alimuona bintiye akiwa mwenye wasiwasi.
"Uko sawa lakini?," Mamake alimuuliza, "au unaumwa popote."
"Mi' niko sawa kabisa ila...," Labibu alisita.
"Ila..."
"Jana tena ndoto ile ikijirudia na mpaka sasa haitoki akilini."
Bi. Tabasuri alishtuka kwa kusikia maneno ya mwanawe, lakini mumewe hakuonekana kuguswa na yale ambayo bintiye alikuwa anazungumzia. Bi. Tabasuri alimwangalia mumewe kwa macho kanakwamba yaliuliza "unafikiri nini kuhusu mambo haya" lakini mumewe hakushughulika naye.
"Binti yangu mpendwa," Bw. Nadama alimuita bintiye.
"Bee," Labibu aliitikia kwa hofu.
"Hakuna haja ya kujiweka mazonge, sababu kama hiyo ndo imefanya niwatoe leo angalau twende tuuzuru mji wetu wa Warsha. Hizo ni ndoto tu, wangapi wameota ndoto za kutisha kuliko yako!"
Masaa yaliwapeleka kwa kasi, walipofika mjini ulikuwa mwendo wa saa sita, wakaingia katika hoteli moja ya kifahari wakajipa cha mchana kisha wakatoka kwenda kufanya shughuli zao. Baada ya kuzunguka kwa muda na kununua vitu vya matumizi, walianza safari ya kurejea nyumbani.
****
Walipoondoka mjini Warsha ulikuwa mwendo wa saa mbili thenashara, Labibu aliangalia nje akafurahia. Kwake, usiku huo jiji hilo lilikuwa zuri zaidi kuliko walipoingia adhuhuri. Aliona watu kila pembe aliyotazama kutoka alipoketi.
"Ni kama ndo kunapambazuka kwa upande wao," alimwambia mamake baada ya kuchunguza manthari yale kwa muda, "panaonekana penye shughuli nyingi."
"Ni kweli usemayo," mamake alimuunga mkono, "mie nionavyo ni kwa sababu wale waliokuwa kazini mchana kutwa sasa ni wakati wanafanya shughuli zao."
"Wengi ambao wako hapa kwa sasa ni vijana," Bw. Nadama aliwajuza, "wamekuja kwa shughuli mbakimbali; wengine wamekusanyika vikundi vidogovidogo wakifanya biashara zisizo halali, wengine hata wana nia ya kuvunja maduka wajipe pesa na wengine wamejibana vichochoroni wakiuza mihadarati."
"Sidhani kama wanaweza kuwa wanauza dawa za kulevya, dawa hizo nasikia ni ghali mno na sitaraji vijana wetu wawe wanafanya kazi hiyo, kazi zao zenyewe ni za mikono, midomo na matumbo yao."
"What if I tell you they are funded."
"By who!"
Bw. Nadama aliliwachia swali la mkewe akapinda njia ya kutoka mjini, nyumbani kwao kulikuwa kama kilomita thelaehini hivi kutoka mjini. Walipobeta na kuchukua njia ya mwituni, moyo wa Labibu ulishtuka mara moja, nywele zikasimama kichwani. Alihisi uoga akaona vyanda vyake vimeroa kwa jasho mara moja na mate kumkauka kinywani.
"Da...d a...a...m fear...ful," alimwambia babake akisitasita, "le...t's not use that route, it m...ay not be safe."
"Huu msitu hauna wanyama pori," babake alimwambia akicheka, "najua unafikiri kwamba wapo."
"Nahisi tu tusiifuate njia hiyo saa hizi, sihisi salama kabisa, kwanza usiku huu tukipatwa na janga katikati ya msitu nani atatuauni!"
"Ni kweli asemayo, hebu fuata anayokuambia kabla hatujapatwa na janga," mkewe alimshauri naye sauti ikimtoka kwa uoga.
Licha ya kuonywa na mkewe pamoja na bintiye, alivimba kichwa akaendelea na safari, mwenyewe alifikiri labda ni uoga wa wanawake. Safari iliendelea shwari ingawa Labibu alipokuwa, moyo ulidunda kwa nguvu kama ulotaka kupasua kifua upate upenyu wa kutoroka. Walipofika katikati ya msitu huo, waliona tumbili wakichupa kutoka mti mmoja mpaka mwingine. Wengine walikuwa wanavuka barabara kwa kasi kama waliotoroshwa.
Kitendo cha wale hayawani kilimuingiza baridi Bw. Nadama, alikuwa amezoea kutumia njia hiyo lakini tabia ya wanyama hao ilimpa wasiwasi.
Akiwa bado amezuba kwa wanyama, mti mkubwa ulianguka mbele yao pap! katikati ya barabara nusra kuangukia gari, alishika breki za ghafla kisha injini ya gari ikazima.
Kutoka walipokuwa wamekwama, kwa mbali wa kama mita thelathini hivi Labibu aliona watu watano hivi waliovalia magwanda mekundu wakiwajia. Kila mmoja wao alikuwa amebeba upanga mkononi, panga zao zilimulikamulika kutokana na mbalamwezi.
"Angalia!" Labibu alimuonyesha babake kwa kidole, sauti ilimtoka kwa wasiwasi.
"Tokeni!" Bw. Vura aliwaamuru akijaribu kufungua mlango wake haraka tena kwa nguvu.
Mama na mtoto walishuka wakatundika miguu begani kuokoa maisha yao. Mlango wa dereva ulikuwa umegoma kufunguka, pale ndani kijasho cha uoga kilianza kumtiririka, alitamani aote mbawa au muujiza utendeke apotee na kutokea kwingine lakini akasalia vile. Mahasidi wake waliookaribia alitambua mmoja wao.
"Nimemfanyia nini kunipangia haya?!" Alijiuliza.
Walipomfikia, kwa ghafla mlango ulifunguka akatoka mbio kama risasi kuwatoroka nduli wale. Wenzake walipoona windo linatoweka walimfuata. Bw. Nadama alijikwa akaanguka, waliokuwa wanamkimbiza walipomfikia walimuinua haraka na kumpigisha magoti magoti, mmoja wao akanyanyua juu upanga tayari kumuangamiza.
"Stoop!" Aliyeinua upanga tayari kumuondoa alisitishwa kwa sauti iliyotokea mitini kama mita ishirini hivi kutoka walipokuwa, "don't kill him."
"Labibu we' nenda," Bw. Nadama alimpazia sauti baada ya kutambua sauti ya bintiye.
"Hapana baba!"
"Go!" Alimuamuru kwa hamaki.
Labibu aliondoka alipokuwa amejificha baada ya kuamrishwa na babake. Bw. Nadama pale alipopiga magoti alijiona katika ndoto ambayo alikuwa amesimuliwa mara nyingi na mwanawe lakini akapuzilia mbali. Yote aliyokuwa akisimuliwa na mwanawe yalikuwa katika hali halisi.
Bi. Tabasuri na bintiye walihangaika ndani ya msitu bila kupata mafanikio ya kuchomoka.
"Did they kill him in your dream?," Bi. Tabasuri alimuuliza mwanawe akimvuta aketi kando yake.
"Kila ilipofika hapo aliponiamuru niondoke ndoto yangu ilikatika kwa sababu nilishtuka kutoka usingizi," Labibu alimwambia mamake, "lakini nafikiri yu' salama."
Pasipo na neno jingine waliinuka wakaanza kuondoka, walizunguka ndani ya msitu mpaka mwishowe wakapata njia ya kuwachomoa walipokuwa wamenaswa.
Walitembea safari nzima kila mmoja akiwa kimya, walipofika nyumbani kwao ilikuwa saa sita za usiku. Walihisi njaa na uchovu juu yake lakini hakuna akiyedhubutu kwenda mapumzikoni. Usingizi uliwapiga chenga. Labibu alikuwa ameketi sebuleni akisafiri katika msongo wa mawazo, Bi. Tabasuri alikaa kando ya mlango akitarajia kusikia mbisho kila sekunde ilipopita. Mwendo wa saa nane, azma yake ilitimia, alishtuliwa kutoka usingizini na ngo! ngo! ngo! mlangoni.
Alipofungua na kumuona mumewe alifurahi, alipoingia ndani neno la kwanza kutoka kinywani lilikuwa jina la rafikiye.
"Vura amefanya nini?," mkewe alimuuliza akimuelekeza sebuleni.
"Alikuwa Kati yao."
"What!"
Mumewe aligeuka na kumwangalia kama aliyekuwa na la kumweleza lakini akasusia, alipoingia na kumuona bintiye alivyokuwa amenywea kitini alimuhurumia. Alimwangalia kwa macho ambayo ni kama yalipitisha ujumbe "niwie radhi, nimejionea mapuuza yangu".