Njiani kuelekea hospitali, Li alileta mazungumzo mepesi akijaribu kumuondoa mama yake Aretha kwenye mashaka. Na mara kadhaa alipojaribu kumuuliza kama Aretha alikuwa na matatizo, alimhakikishia kuwa Aretha hana matatizo zaidi ya daktari kumpa mapumziko ili apate nguvu,
"Unajua mama hii wiki imekuwa na ratiba ngumu sana kwa Aretha, na tukio la leo limezidisha uchovu kwake. Daktari amempa mapumziko na ameshauri uwepo kuongea nae"
"Aaaaah kumbe ndio hivyo, basi nilipata wasiwasi kweli nikadhani amepata ajali" mama akashusha pumzi na kutuliza mwili wake vyema kwenye kiti,
Frans aliyekaa nyuma akatabasamu baada kuona mama yake amekuwa na utulivu.
*************
Edrian alikaa nje ya chumba ambacho Aretha alipelekwa baada ya kutoka Chumba cha Dharura. Alizungumza na Captain kuona namna anavyoweza kudukua taarifa zote kumhusu BM. Akampigia Joselyn
"Hello babe" Lyn akaitika kwa uchangamfu
"Lyn, kama ni wewe umefanya vile kwenye zile picha, nakupa nafasi ukiri mwenyewe. Mara nitakapoju__"
"Babe unaongelea nini mbona sikuelewi" Lyn akashtuka akimkatisha Ed
"Lyn, unajua sijui kufanya utani. Nitafute ukiri na usisubiri nijue mwenyewe" akakata simu pasipo kusubiri Lyn ajitetee
Akaangalia kwenye simu yake video aliyotumiwa na Captain ambayo aliidukua kwenye CCTV za ukumbi wa Southern Pole wakati wa onesho. Akaangalia sana kila mtu aliyekuwepo ukumbini akijaribu kumtafuta BM amuone lakini akashtuliwa na sauti ya Li ambaye aliongozana na mama yake Aretha
Akasimama ili kumsalimia mama, lakini yeye akamuwahi
"Mwanangu sasa mbona wewe ndio unaonekana mgonjwa?" Akauliza mama yake Aretha akijaribu kuweka tabasamu jepesi usoni ili kumpa nafuu Ed. Kwa namna alivyoonekana mama aling'amua hali ya Aretha ilimchanganya sana Ed, naye hakutaka kumpa wasiwasi kwa kuonekana kushtuliwa na jambo hilo.
"Hapana mama, niko salama, samahani sikuweza kuk__"
"Mwanangu usihofu, ndio maana ikaitwa dharura!"
Edrian akajaribu kutabasamu, akawafunguliwa mlango akiwapisha mama na Frans waingie, lakini yeye hakuingia wala Li. Kabla ya kuufunga mlango mama yake Aretha akamwambia kwa sauti ya kunong'ona
"Mbona unarudi nje mwanangu?"
"Nimetoka humo muda si mrefu mama." Akaamua kuupindisha ukweli, Dokta Brianna alimwambia ampe muda Aretha aweze kuchukuana na uzito wa matukio ambayo hayakuwa maisha yake hapo mwanzo. Akakumbuka maneno yake
"Rafiki yangu, huyu binti hajui namna ya kukabiliana na mambo ambayo wewe umeyazoea. Amekuwa akijiepusha na mambo yanayompa changamoto. Mpe muda wa kufikiri vyema, atakutafuta. Nimejaribu kumwambia uwepo wako lakini amenisisitiza anataka uende tu nyumbani hajisikii kukuona kwa sasa"
Edrian akashusha pumzi baada ya kufunga mlango akiwaacha mama na Frans walioingia ndani. Akarudi kuketi alipokaa mwanzo huku Li akiwa pembeni yake
"Bro, mbona uko huku nje?" Uvumilivu ukamshinda Li alipoona kaka yake akishusha pumzi na kuketi kwenye benchi lililokuwa pembeni ya mlango wa kuingia. Uso wa kaka yake ulikosa nuru yake ya kawaida, alionekana kuchoka na hisia zake kuwa katika huzuni.
Edrian akamwangalia Li na kumuuliza "Unadhani kuna namna Aretha ananilaumu kwa yake yaliyotokea?"
Swali hili likamshtua Li, naye akamrushia swali kwa haraka "Kwa nini akulaumu bro"
Akachua paji lake la uso kwa kidole gumbe na vingine viwili akijaribu kuipinga hoja hiyo mwenyewe, "atakuwa vizuri tu baadae, nisifikiri vinginevyo" akawaza.
"Nadhani amechoka tu" akajibu kwa ufupi Ed huku akirudi kuangalia kwenye simu yake.
Li hakuridhika na jibu lile na kwa haraka akahisi huenda Aretha alimlaumu wazi kaka yake
"Bro unamaanisha Aretha anadhani ni
wewe ndio umekwamisha tukio?"
"Nooooo" kwa haraka Ed akamjibu
"Sasa kwa nini hauingii ndani bro?" Li naye akamuwahi kwa swali
"Aaahm sababu akiniona analia zaidi" akajibu kwa sauti ya chini!
"Analia akikulaumu au kitu gani kinapelekea hivyo?" Li akauliza zaidi na sura yake ikawa makini kumtazama Ed
"Arrrrrgh....Li ungesomea tu upelelezi maana una maswali" Ed akalalamika na kuangalia simu yake
"Okay bro sitauliza. Ila nitamkabili Aretha mwenyewe aniambie kama amekuzuia usiingie ndani"