Ed aliondoka kwa hasira ofisini kwake akaelekea kwenye chumba cha mazoezi, ambapo hakusubiri abadilishe nguo akaenda kwenye mashine ya kukimbia.. akiwa na simu yake mkononi meseji ikaingia tena... akakumbuka hakujibu ujumbe wa kwanza alioutuma Aretha ambao alimsalimia, sasa alipousoma huu wa pili, Aretha alikuwa kaandika hivi:
"Nisamehe pia nililala mapema hata ulivyojibu sikusikia.. Is your morning good?"
"Usijali Retha, samahani nami nilikuwa nina kazi ndogo nikachelewa kukujibu. My morning is good, How are you?"
'Ed unajidanganya na unamdanganya Aretha, morning yako imeingiliwa na Joselyn.. he he he..'Ed akajicheka.. na uso wake ulioingia mle chumbani ukiwa umejikunja ghafla mikunjo ikaondoka. Li akayaona mabadiliko hayo ya ghafla lakini akaamua kutoingilia mambo ya kaka yake, alijua kabisa kaka yake alikuwa uncomfortable kwa ujio ule. Akanyamaza na kumuacha kaka yake ashughulikie mambo yake..
Akawasha mashine na kuanza mazoezi akijaribu kusafisha mawazo yake ambayo asubuhi hii yamepitia myumbo wa kila namna. Akawaza ni nini atafanya kujiondoa kwa hili zimwi linalomjua... akaazimu moyoni kumkabili Lyn jioni..
Alipomaliza ilikuwa tayari saa kumi na mbili akachukua taulo na kufuta jasho. Akapanda kuelekea chumbani kwake, lakini akaamua aangalie ofisini kwake kama Joselyn atakuwa ameondoka. Akamkuta kalala vyema kwenye kochi huku sehemu ya blauzi yake ikiwa imepanda juu na kusababisha tumbo lake kuwa wazi.. Akataka kumuamsha lakini akaangalia muda akajua atachelewa kazini iwapo ataanza tena kubishana na Lyn.
Akageuka na kuurudisha mlango akaelekea chumbani huku akijibu ujumbe wa simu ulioingia...
Alipomaliza kuoga na kuvaa, akatoka tayari kuelekea kazini. Akaamua kwenda kumuamsha Lyn.. lakini jitihada zake zilipotea zote baada ya Lyn kumwambia amuache alale ataondoka akiamka..
Ed akaamua kuondoka japokuwa bado alikuwa na wasiwasi na kile ambacho Lyn angeweza kufanya ofisini kwake. Pia hakutaka aingie chumbani kwake.
Alipokuwa akishuka ngazi Zena mhudumu wao nae akawa akipanda ngazi huku mkononi akiwa na begi dogo
"Kaka Ed, Jere kasema nilete ndani begi hili ni la Dada Lyn, niweke chumbani kwako au chumba cha wageni" swali hili lilimtoka Zena sababu ni kawaida mara zote Lyn alipokuja kulala, Ed alimwambia aandae moja ya chumba cha wageni ambacho kilikuwa karibu na chumba chake. Lakini leo begi lilimfanya ashtuke na kufikiri labda Lyn alikuja kuishi pale
Ed ambaye wakati huu alisimama ili kumsikiliza Zena, akashusha pumzi kuonesha kutojua kabisa nini ajibu sababu ujio wa Lyn sasa unaleta maswali magumu ya kujibu..
"Mmmm" akaguna kama kawaida
"Usijali Zena nipe hapa nitalipeleka mimi' sauti ya Li kutoka nyuma ya Ed ilimjibu
Ed akageuka, akampa ishara ya asante Li, akashuka na kwenda kazini huku akijua Coletha atakapomuona Lyn utakuwa ni uwanja wa panya na paka..
Akaingia kwenye gari na kuondoka akiyaacha yaliyomsibu asubuhi ile nyuma ya kichwa chake.. "There is too much work today" akajisemea
Akiwa njiani akaamua kumpigia Coletha ili kumtahadharisha uwepo wa Lyn na kumsihi wasianzishe mtafaruku. Coletha akamhakikishia kaka yake kuwa hatosababisha shida.
Asijue, Coletha naye alikuwa na mpango wa kuwa karibu na Aretha ili kujua kwa nini kaka zake yaani Li na Derrick ni kama wana mbinu za kuwafanya Ed na Aretha kuwa wapenzi, Lyn hakuwa tatizo lake tena... alijua kama kweli kaka yake atampenda Aretha hahitaji kupambana na Lyn.
"Usihofu bro, nitakushangaza" Coletha akamjibu kabla ya kukata simu.
************************
Joselyn alipofumbua macho alikuwa amelala kitandani japokuwa hakuwa amevua viatu wala nguo alizovaa. Akakumbuka alilala kwenye kochi ofisini kwa Ed... "nani alinileta hapa?" Akajiuliza
Akatabasamu akifikiri atakuwa ni Ed ndio aliyembeba hadi kumleta chumbani... akarudi kulala akiwa na shauku ya kumuuliza Ed....
Akaangalia pembeni akaliona begi lake...akachukua simu na kumpigia Ed ambaye hakupokea...
"Am sorry babe, wivu wangu ndio unanifanya nafanya ninayofanya, I love you Edrian" akamtumia Ed.
Kisha akainuka na kufungua mlango huku akiita kwa sauti...
"Zenaa" akaita